PENZI TAMU[I]

Tukusuma Mpoki alikuwa amesimama kwenye baraza la nyumba yake, uso wake ukiwa umekunja ndita, jasho likimtiririka, na macho yake yakiwa yanabubujikwa na machozi. Alikuwa amejifunga kanga moja tu kati ya eneo la kifuani na kiunoni na hivyo kuonesha mapaja yake yaliyonawiri vizuri na hivyo kulidhirisha kwa kadamnasi umbo lake lake la nyigu. Chini ya kanga hiyo alikuwa amevaa chupi ya rangi nyekundu. Licha ya upepo wenye joto la jiji hilo la bandari salama kumpulizikia bila kukoma Suma aliendelea kusimama kwenye baraza la nyumba hiyo. Hakujali watu waliokuwa wamesimama upenuni wakimshangaa binti huyo wa Kinyakyusa akiwa katika hali ya hasira na aliyekuwa akipaza sauti yake akimtukana mumewe bila kufunga breki. Mkono wake wa kushoto uliokuwa umevikwa bangiri za rangi ya dhahabu ulikuwa umekunjwa kwenye kiwiko na kuegeshwa kama gari la kijapani kwenye kiuno cha binti huyo kilichokuwa kimehifadhi vyema mviringo wa makalio yake uliokuwa kama vitunguu maji vinavyolimwa kule Tukuyu.

Mkono wake wa kulia ulikuwa umeinuliwa juu, huku kidole cha kati kikining’inia hewani utadhani kimepigiliwa msumari katika staili ya kumzodoa mtu. Kucha zake ndefu zilizopakwa rangi nyekundu inayong’ara zilionesha ni jinsi gani Suma (kama alivyozoea kuitwa mtaani) alivyokuwa anajijali. Nywele zake ndefu zilizosukwa kwa mtindo wa rasta zilining’ia mabegani kama nywele za simba jike. Suma alikuwa amekasirika, na hasira yake ilionekana wazi siku hiyo. Hakuna aliyewahi kuhisi kuwa dada huyo anaweza kuweza kumpaka mtu hadharani namna hiyo.

“Toka hapa, unadhani mwanamme peke yako” Alifoka binti huyo huku sauti yake yenye lafudhi ya mbali ya kinyakyusa ikipasua anga la eneo hilo la Chang’ombe.

“Yaani kukupenda wewe ndio imekuwa nongwa, mwanamme gani huridhiki, kama penzi langu hulitaki si uende huko huko ulikolala jana, firauni mkubwa, kama unafikiri huyo malaya wako anaweza kukupenda kama nilivyokupenda sasa mbona umerudi hapa?” Aliendelea kubwata bila hata ya kumeza mate. Sauti yake ikiwa kavu na isiyoonesha kujali nani anasikiliza au nani anamuangalia. Watu walifurahia sinema hiyo ya bure.

Hatua kama kumi hivi toka mlango wa nyumba yake ambayo ilikuwa ni ya mwisho ikipakana na nyumba za Polisi za Chang’ombe alikuwa amesimama Sospeter Mkiru, mdomo umemdondoka utadhani amemuona mzee Ole wa Usiku wa Balaa, na mkononi akiwa bado ameshikilia shati la lilikuwa limechanika mgongoni baada ya Suma kulishindilia kucha za uhakika.

“Jamani Suma nisamehe mpenzi sitarudia tena” Alisema Sosi huku maneno yake yakitoka kwa kukwamakwama kama maji yanavyotoka kwenye mpira wa kumwaligia maua. Soni zilimshika. Alijikaza kisabuni huku akibembeleza apewe nafasi nyingine.

“Nikusamehe mara ngapi nyang’au mkubwa we!” Dada Suma utadhani ametiwa ufunguo aliendelea kumpaka. “Jamani hata uvumilivu una mwisho. Mimi sasa basi, nenda huko unakokwenda kila siku utanletea magonjwa bure miye”

“Tafadhali Suma nisamehe mke wangu” Sosper alianguka na kupiga magoti kwenye mchanga uliokuwa unajoto. Alijaribu tena kumbembeleza binti huyo.

“Nenda kafilie mbali, hayawani mkubwa” Suma alisema huku akimwelekeza Sosi kwa kidole kuondoka hapo. Hayo yalikuwa ni maneno ya mwisho ambayo Sospeter aliyasikia toka kwa Suma Mpoki. Alimuona Suma akigeuka na kuelekea ndani ya nyumba.

Sosi alijua kuwa safari hii amevurunda kweli kweli. Uchungu ulianza kumpanda pole pole na donge la hasira ya kumpoteza waridi lake na mpenzi wake wa toka shule lilimkaba shingoni. Alijihisi kuwa amejidhulumu penzi na anastahili adhabu hiyo kali. Alitamani amkimbilie Suma na kujiangusha miguuni mwake na kumwomba radhi huku akijigaragaza. Akili yake ilianza kwenda kwa kasi akijiuliza ni shetani gani lilimwingia hadi kumfanya kwenda kulala na mwanamke waliyekutana kilabuni na kumuacha mpenzi wake wa damu? Alijihisi kizunguzungu. Kama mtoto mdogo Sosi aliunganisha vidole vya mikono yake kichwani huku shati lake akilibeba begani. Watu waliokuwa wamesimama kushuhudia tukio hilo walianza kujipangua taratibu huku wengi wakimuonea huruma Sospter na wengine wakisema wazi kuwa “amejitakia” mwenyewe. Wachache hawakuficha dhihaka yao kwani walimcheka hadharani na kumuona kweli huyo jamaa wa kuja. Sospeter aliapa hatarudi tena mitaa hiyo kwa aibu aliyoipata Chang’ombe. Akiwa haangaliki anakokwenda, Sosi alijikuta yuko katikati ya barabara ya Chang’ombe huku magari yakijaribu kumkwepa, na watu wakimrushia matusi ya kila aina hata matusi yasiyosajiliwa. Gari aina ya Fuso ambalo lilikuwa limeshehena mashabiki wakitoka uwanja wa Taifa lilijitahidi kufunga breki na kumkwepa kwa ustadi mkubwa. Sauti ya breki zake ziliumiza masikio ya watu. Mlio wa mshtuko wa watu ulitanda angani, huku watu wakishika vichwa vyao na wengine kufumba macho wasione kile kilichokuwa kitokee.. Sospeter hakupata nafasi ya kukwepa Fuso hilo, kwani alirushwa juu kama kopo tupu la kimbo. Alipotua kwenye lami yenye mashimo mashimo, mwili wake ulikuwa hauna ishara yoyote ya uhai ndani yake. Watu walikimbilia hapo kuangalia kilichotokea, huku kina mama wakipiga kelele ya kilio wakiwaficha watoto wao wasishuhudie jambo hilo.

Bila kusogea hata sentimeta moja, Suma alijisemea moyoni “Ukome!” Suma aligeuka kwa haraka huku akiangua kilio alichokuwa amekizuia kwa muda na kuingia ndani ya nyumba ambayo alikuwa anaishi na wadogo zake. Mwili wote ulikuwa unamtetemeka huku hisia ya furaha ya kisasi na hatia ya uovu vikimkaba rohoni. Moyo wake ulikuwa umejeruhiwa kwa mapenzi na kumbukumbu ya mapenzi ilimuumiza mtima. Alijihisi amepoteza muda mrefu na kijana Sospeter ambaye walikuwa wakiishi kama mume na mke. Alijidharahau na kujiona kweli “amepatikana” kwa kukubali penzi la kijana huyo chakaramu. Aliapa moyoni mwake kuwa hatopenda tena, kwani wanaume ni kama mbwa. Aliendelea kulala kitandani huku ameukumbatia mto huku moyo wake ukipaza sauti ya kilio chake mbele za Mungu. Aliendelea kulia hadi alipopitiwa na usingizi huku akiwaza jinsi alivyokutana na Sosi kwa mara ya kwanza.

Comments

Popular posts from this blog

Vifahamu Vitu Vidogo Vidogo Ambavyo Huzidisha Utamu wa Mahusiano Katika Mapenzi

UTAMU WA MCHEZO SEHEMU YA 2

Jinsi ya kumtoa msichana Bikra bila maumivu, wengi hawajui hili, Cheki hapa.